Exodus 34

Vibao Vipya Vya Mawe

(Kumbukumbu 10:1-5)

1 a Bwana akamwambia Musa, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitaandika juu yake maneno yale yaliyokuwa kwenye vile vibao vya kwanza, ulivyovivunja. 2 bUwe tayari asubuhi, kisha upande juu ya Mlima Sinai. Uje mbele zangu kukutana nami huko juu ya mlima. 3 cMtu yeyote asije pamoja nawe, wala asionekane mtu popote juu ya mlima, wala kondoo na mbuzi au ng’ombe wasilishe karibu mbele ya huo mlima.”

4 dKwa hiyo Musa akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, naye akapanda juu ya Mlima Sinai asubuhi na mapema, kama Bwana alivyokuwa amemwagiza, akachukua vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. 5 eKisha Bwana akashuka katika wingu akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina lake, Bwana. 6 f Bwana akapita mbele ya Musa, akitangaza, “Bwana, Bwana, Mungu mwenye huruma na neema, asiye mwepesi wa hasira, mwingi wa upendo na uaminifu, 7 gakidumisha upendo kwa maelfu, pia akisamehe uovu, uasi na dhambi. Lakini haachi kuadhibu mwenye hatia; huwaadhibu watoto na watoto wao kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata katika kizazi cha tatu na cha nne.”

8Mara Musa akasujudu na kuabudu. 9 hMusa akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”

Kufanya Agano Upya

(Kutoka 23:14-19; Kumbukumbu 7:1-5; 16:1-17)

10 iKisha Bwana akasema: “Tazama ninafanya Agano mbele ya watu wako wote. Mbele ya watu wako wote nitafanya maajabu ambayo hayajafanyika katika taifa lolote katika ulimwengu wote. Watu wale mnaoishi miongoni mwao wataona jinsi ilivyo ya kushangaza ile kazi nitakayowafanyia mimi Bwana wenu. 11 jTii yale ninayokuamuru leo. Tazama nawafukuza mbele yako Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 12 kUwe mwangalifu, usifanye agano na wale wanaokaa katika nchi ile unayoiendea, la sivyo watakuwa mtego katikati yako. 13 lBomoa madhabahu yao, vunja mawe yao ya kuabudia na ukatekate nguzo zao za Ashera. 14 mUsiabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni Wivu, ni Mungu mwenye wivu.

15 n o“Uwe mwangalifu usifanye agano na wale watu wanaoishi katika nchi, kwa maana wakati wanapojifanyia ukahaba kwa miungu yao na kuwatolea kafara, watakualika wewe nawe utakula sadaka za matambiko yao. 16 pUnapowachagua baadhi ya binti zao kuwa wake wa wana wenu na binti hao wakajifanyia ukahaba kwa miungu yao, watawaongoza wana wenu kufanya vivyo hivyo.

17 q“Usijifanyie sanamu za kusubu.

18 r“Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, kama nilivyokuamuru. Fanya hivi kwa wakati ulioamriwa, katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa kuwa katika mwezi huo ndipo wewe ulipotoka Misri.

19 s“Mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo ni mali yangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wote wa kiume wa mifugo yako, ikiwa ni wa ng’ombe au wa kondoo au mbuzi. 20 tUtakomboa mzaliwa wa kwanza wa punda kwa mwana-kondoo, lakini kama humkomboi, utavunja shingo yake. Utakomboa wazaliwa wako wa kwanza wote wa kiume.

“Mtu yeyote asije mbele zangu mikono mitupu.

21 u“Kwa siku sita utafanya kazi, lakini siku ya saba utapumzika, hata ikiwa ni majira ya kulima au ya kuvuna lazima upumzike.

22 v“Utaadhimisha Sikukuu ya Majuma kwa malimbuko ya mavuno ya ngano, na Sikukuu ya Mavuno mwishoni mwa mwaka. 23 wMara tatu kwa mwaka wanaume wako wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi, Mungu wa Israeli. 24 xNitawafukuza mataifa mbele yako na kupanua mipaka ya nchi yako, wala hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yako wakati unapokwenda mara tatu kila mwaka kuonana na Bwana Mwenyezi Mungu wako.

25 y“Usinitolee damu ya dhabihu pamoja na kitu chochote chenye chachu, wala usibakize dhabihu yoyote ya Sikukuu ya Pasaka mpaka asubuhi.

26 z“Leta matunda ya kwanza yaliyo bora zaidi ya ardhi yako katika nyumba ya Bwana Mwenyezi Mungu wako.

“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.”

27 aaKisha Bwana akamwambia Musa, “Andika maneno haya, kwa maana kulingana na maneno haya, nimefanya Agano na wewe pamoja na Israeli.” 28 abMusa alikuwa huko pamoja na Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya Agano, yaani zile Amri Kumi.

Mng’ao Wa Uso Wa Musa

29 acMusa alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa uking’aa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Bwana. 30Haruni na Waisraeli wote walipomwona Musa, kuwa uso wake unang’aa, waliogopa kumkaribia. 31 adLakini Musa akawaita, kwa hiyo Haruni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao. 32 aeBaadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zote Bwana alizompa katika Mlima wa Sinai.

33 afMusa alipomaliza kuzungumza nao, akaweka utaji kwenye uso wake. 34Lakini kila wakati Musa alipoingia mbele za Bwana kuzungumza naye, aliondoa ule utaji mpaka alipotoka nje. Naye alipotoka nje na kuwaambia Waisraeli lile ambalo ameagizwa, 35waliona kuwa uso wake unang’aa. Kisha Musa angeliweka tena utaji juu ya uso wake mpaka alipokwenda kuzungumza na Bwana.
Copyright information for SwhKC